TUNZA NDOA YAKO

Sehemu ya Pili

Na Aloyce Kalunde

Ukhali gani msomaji wa makala hii, nishukuru kwanza kwa wote mliotuma maoni yenu kwa email na simu. Maoni yenu nishayafanyia na ninaendelea kuyafanyia kazi.  Ungana name sasa hasa kwa kuchambua:

KANUNI ZA MSINGI KATIKA NDOA

Mungu ndiye mwanzilishi wa ndoa ambaye alifunga ya Adamu na Hawa katika bustani ya Edeni (Mwa.2:18-24). Tukitaka kuelewa muungano huu wa mume na mke ni muhimu tuelewe kanuni za msingi za kibiblia. Kuna maneno matatu ambayo ni muhimu tuangalie kwa kifupi maelezo yake.

1.     Kuondoka (leaving).
Hii humaanisha kuwa wanandoa yaani mme na mke, wote wawili huhitaji kuamua nyumba na familia yao ni kwao wawili tu, hata kama wanahitajika kuwaheshimu wazazi na jamaa wote wa pande zote mbili. Tangu siku ya kufunga ndoa wote wawili wafahamu kuwa mahali pa kwanza pa kupata msaada na ushauri ni kutoka kwa mwenzi wake. Mume na mke wanakuwa na umoja mkamilifu. Wajibu wao wa kwanza unakuwa kwao wenyewe. Wanapooana kipaumbele ni kwa mke au mume wa kwanza.

2.     Kuambatana (cleaving).
Neno hili linatokana na neno la Kiebrania ‘dabag’ lenye maana ya kushikamana na mwenziwako wa ndoa na kuwa kitu kimoja. Neno hili ni zito sana katika maana yake ya asili, yaani Kiebrania. Humaanisha kugandamana, kushikamanan au kung’ang’aniana kama stempu inavyogandamana na barua. Ukijaribu kutenganisha stempu na barua vyote huchanika na kuharibika. Kimatendo inamaanisha kuwa na uamuzi wa kumchagua mwenzi wako kuwa rafiki na mpenzi wako na anakuwa wa kwanza wa kushauriana naye.

Kuambatana ni kujitoa kabisa kwa mwenzio. Hili lina maana ya ahadi, uhakikisho kwa mwenzio. Kwa hiyo kuambatana ni uamuzi wa dhati na wa kukusudia ili kutengeneza muungano. Ndoa yenye afya ni ile ambayo ina muungano sahihi uliotokea kati ya mwanamke na mwanaume.

3.     Kuwa mwili mmoja (one flesh).
Kuwa mwili mmoja maana yake ni kuwa na upendo wa ndani na kuunganika katika hisia, utu, na ushirika mtakatifu wa tendo la ndoa (1Kor.6:16; 7:2-5). Hili linahusu hasatendo la ndoa. Kujamiiana kwa wanandoa ni kitu kitakatifu na mapenzi ya Mungu.

Yapo mambo mengi ya muhimu watu wanapokuwa mwili mmoja: Kuleta umoja wa nafsi na roho. Tendo la ndoa katika mwanadamu hugusa kila sehemu ya utu wake. Kufanyika mwili mmoja haihusishi tu hali ya mwili, bali hisia na roho kwa kifunganisho cha ukaribu wa faragha. Pia tendo hilo huongeza furaha kwa wapenzi hao wawili.


ZIJUE TOFAUTI KATI YA MUME NA MKE (GENDER DIFFERENCES)
Kuna ukweli kwamba mwanaume na mwanamke wanaweza wasijuane hali zao za tofauti kijinsia katika maisha yao na ikabaki kuwa ni siri. Inawezekana ni namna ambayo Mungu ameifanya, vinginevyo maisha yangekuwa ni kitu cha kuchosha sana kwa mwanadamu bila kuwa na kazi ya kutaka kugundua mambo mapya.

A.   Tofauti katika mawasiliano
        1. Wanawake:
Þ   Wanawake wana uwezo mkubwa wa kuhisi mambo au hali halisi ya jambo fulani (jema au baya) kuliko wanaume. Ndiyo maana inaaminika kuwa wanawake wanamilango sita ya fahamu.

Þ   Katika mazungumzo wanawake hupenda kuzungumzia mambo yanayo gusa hisia, mahitaji, matumaini, ndoto, mambo yanayoleta hamu (wants), shida mabalimbali, suluhisho katika shida na mambo yoyote yanayo husu mahusiano. Wanawake hutaka wanaume wawasikilize na kuwajibu. Hupenda waume zao wawaone ndani ya mioyo yao na fahamu zao (minds) na kisha kujua kile kinachowafanya wafurahi au wawe na huzuni. Wanawake humtaka mwanaume ambaye atajitoa kwake siku zote za maisha yake, anayetunza uaminifu kama jiwe kuu la pembeni la uhusiano. Wanapenda mwanaume anayefurahia maisha pamoja nao, anayejua kucheza, aliyetayari kujiona kuwa anao upungufu mahalifulani. Wanamtaka mtu aliye mbunifu, asiye mwoga, mwenye akili na mwajibikaji katika maisha yake.

Þ   Mwanawake anamtaka mume aneyeweza kujalimahitaji yake kwa undani sana, atakaye tambua mahitaji yake, aliye wazi katika msimamo wake.


Þ   Wanawake kwaasili ni watu wa kupenda na ni wasiri. Waandishi mbalimbali, washairi na wanasaikolojia waliojaribu kulijibu swali gumu katika kutafakari juu ya wanawake huhitaji nini hasa, bila mafanikio.

Þ   Mwanamke ni kiumbe wa ajabu (complex and intricate being). Mwanamke anahitaji shukrani toka kwa mumewe anapofanya jambo jema. Wanawake ni watu wa hisia za ndani sana, huguswa na kila jambo linalofanyika.

Þ   Wanawake hujihusisha zaidi na kutengeneza mahusiano ya karibu ambayo yanashikiliwa pamoja na hali ya kiunganishi. Hii inamaana wanawake wanafurahia katika hali ya kuunganika na kuambatana katika mahusiano. Kwa maana nyingine wanawake hufurahia kuwa na mahusiano ya ndani. Hii ndiyo sababu umuhimu wa kuolewa kwa wanawake ni suala la kipaumbele kwa sababu utambulisho wa mwanamke unapatikana katika muunaganiko wa mahusiano. Wanawake huolewa kwa lengo la usalama na kupata watoto.

Þ   Wanajisikia vizuri kuwa wanawake.

2.   Wanaume
Þ   Wanaume hupenda wanawake wenye kuwahudumia na kuwafariji, wenye kujishusha, wasiojikweza au kuhukumu, wenye ujuzi wa maisha.
Þ   Hupendelea mwanawake anayevutia. Kwa kawaida mwanaume husisimuliwa kimapenzi kwa kumwangalia mwanamke kwa macho. Hivyo hupenda mke wake awe katika mwonekano mzuri na wa kuvutia.
Þ   Hitaji la msingi la mwanaume ni kutoshelezwa katika tendo la ndoa. Inasemekana kitaalam kuwa mwanaume akikaa muda mrefu bila kufanya tendo la ndoa toka kwa mke wake mambo yafuatayo yanaweza kutokea:
Ø Mume kushindwa kuongea kwa uchangamfu kama alivyo zoea.
Ø Mume kuumwa kichwa na kupata homa.
Ø Mume kuwa mkali nyumbani na nje.
Ø Hukosa hamu ya kula.
Ø Anaweza kuwa na ugonjwa wa tumbo kushika, kukosa haja kubwa.
Ø Kuwa na ugonjwa wa mapigo ya moyo, kushuka au kupanda kwa sababu ya mawazo mengi ambayo hawezi kuyaeleza wazi wazi.
Ø Anaweza kumsingizia mke wake na kumpa majina ya ajabu na kumdhalilisha mbele za watu.
Ø Mume anaacha kutoa mahitaji ya nyumbani mwake kwa kutaka kumkomoa mke wake.
Ø Mwili wa mwanaume hutengeneza mbegu za kiume ambazo zimechanganyikana na madini ya chokaa (calcium). Chokaa inapolundikana bila kupata njia sahihi ya kutoka yaani ya tendo la ndoa, husababisha mrija wa haja ndogo (urethra) kubanwa hata kuziba. Matokeo mwanaume hupata ugonjwa wa mshipa au ugonjwa wa wazee.
Ø Mume bila mwili wa mke wake kwa muda mrefu akili zake si timamu, akili zake hazitafanya kazi vizuri.
Ø Sukari mwilini kupanda na kushuka.
Þ   Wanaume si watu wa mahusiano kama wanawake.
Þ   Wanaume ni watu wanaoshughulika na vitu, shughuli nyingi na mipango mingi ya kazi. Si watu wa kuonyeha hisia zao kwa wepesi.
Þ   Wanaume hujiona kukomaa wakati wanaweza kujitenganisha wenyewe kama watu binafsi. Huwa wanathamini kuwa huru na kuwa na utawala kama njia ya kujisikia kukamilika na kuweza kutembea kwa ujasiri katika maisha.

B. Tofauti katika mahitaji makuu

Yako mahitaji mengi sana ya muhimu kwa wanandoa, lakini katika hayo yapo yaliyo ya msingi zaidi ambayo hutofautiana kati ya mwanaume na mwanamke katika vipaumbele.
1.     Wanaume
*    Kutoshelezwa katika tendo la ndoa.
*    Rafiki wa kustarehe naye.
*    Mwenzi au mke anayevutia.
*    Msaada wa mambo ya nyumbani.
*    Kuheshimiwa na kuthaminiwa.

2.     Wanawake
·        Kupendwa kwa upole.
·        Maongezi ya kirafiki.
·        Uaminifu na uwazi.
·        Msaada wa kifedha.
·        Kujitoa katika familia.

KANUNI ZA NDOA NA NYUMBA
Kwa kuwa ndoa ni mahusiano kati ya mume na mke ni muhimu kutunza ili izidi kudumu. Zifuatazo ni amri kumi kwa kila mwanachama.

A.   Amri Kumi za Mwanamke.
1.     Mpende Bwana Mungu kwa moyo wako wote, kwa akili zako zote, nafsi yako yote na kumpenda mume wako kwa nguvu zako zote ila isiwe kama umpendavyo Mungu wako (Kumb.6:5).
2.     Kwa furaha mtii mume wako kama kumtii Kristo (Efe. 5:22).
3.     Fanya bidii kuutawala ulimi wako, kuwa mwangalifu mbariki nakumtia moyo mume wako. (Mith. 31:26).
4.     Fanya bidii kujitunza na nyumba yako ipendeze na kuvutia (Mith.31:27, 28).
5.     Tunza furaha ya moyoni katika ratiba ya siku nzima kwa kazi ulizo nazo (Kol. 3:17).
1.     Usiruhusu wivu na uchoyo kuwa asili yako (Mith.6:34).
2.     Mpende mume wako wala usimlinganishe na wengine, kwa uaminifu mwitikie na kumheshimu (Efe.5:33).
3.     Mtukuze Mungu kule kuitwa mwanamke na uzuri wa thamani hiyo kuliko maisha yenyewe (Mith.12:4).
4.     Pandikiza kwa watoto wako upendo, heshima na adabu kwa baba yao (Mith.  22:6).
5.     Usihofu makosa na kukosea (Mith. 24:24; 27:15).

B.   Amri Kumi za Mwanaume
1.     Mpende mkeo kama Kristo alivyolipenda kanisa, uwe tayari kuutoa uhai wako kwa ajili yake ili aweze kukua katika Kristo (Efe. 5:25).
2.     Mfikirie na kumtia moyo kwa kuwa Mungu hakumkusudia wajibu mzito (1Pet. 3:7).
3.     Kamwe usiwe na uchungu moyoni kwa maakosa ya mke, bali msamehe kama Kristo alivyokusamehe wewe (Efe. 4:32).
4.     Mwongoze mke wako na familia katika njia za haki, waambukize maisha ya kiroho na hofu kwa Mungu (Efe.5:22).
5.     Uwe kichwa cha familia, ili uwapatie ulinzi unaotakiwa, upendo na ulinzi wa kibaba kama Mungu alivyokusudia (1Kor. 11:3).
6.     Ishi kwa furaha na mke wako ukijua huyo ni zawadi kwako kutoka kwa Mungu (Mwa. 2:18).
7.     Mbariki, mtukuze na kumsifu mke wako, kwamba hakuna kama yeye duniani (Mith. 31:28, 29).
8.     Mwamini mkeo ili kwamba yeye awe mke ambaye Mungu anataka uwe naye (Mith. 31:11).
9.     Kwa upendo mwambie mke wako matakwa yote kwa kufanya kwa matendo, hivyo onyesha shukrani zako kwake (Efe. 4:29).
10.                        Jitunze mwenyewe kwa ajili ya mkeo, jitolee mwenyewe kwake tu (Rum.12:10).

Toa maoni yako kupitia
Email:Kalunde47@gmail.com
+255 783 700083
+255 653 700083


Comments